Juhudi za kufikia usitishaji mapigano nchini Lebanon zimeongezeka zaidi ya saa chache zilizopita, kwa mujibu wa ofisi ya Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati, na kuongeza kuwa mawasiliano kati ya Marekani na Ufaransa yanaendelea ili kufufua pendekezo la kusitisha mapigano kati ya Hezbollah na Israel.
Rais wa Marekani Biden na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron walipendekeza kusitishwa kwa mapigano kwa siku 21 wakati wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi uliopita.
Israel ilimuua kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah siku tatu baada ya pendekezo hilo na kuanzisha mashambulizi makali dhidi ya kundi hilo, na hivyo kusambaratisha mazungumzo hayo.
Netanyahu alikataa hadharani kusitisha mapigano kabla ya mauaji hayo.
Matarajio ya mapatano yalipungua zaidi baada ya Iran, ambayo inaunga mkono Hezbollah, kurusha safu ya makombora dhidi ya Israeli wiki iliyopita.
“Kuna mawasiliano yanafanyika kati ya Marekani na Ufaransa…kwa lengo la kufufua tamko la kusitisha mapigano kwa muda maalum ili kuanza tena kutafuta suluhu za kisiasa,” ofisi ya Mikati ilisema kwenye X, ikimnukuu waziri mkuu