Katika hotuba yake ya kwanza kabisa tangu atangazwe mshindi wa uchaguzi wa Liberia, rais mteule Joseph Boakai, amemsifu rais George Weah, kwa kukubali kushindwa baada ya muhula mmoja pekee madarakani.
Aidha aliongeza kuwa, ameunda timu yake ya mpito ambayo itafanya kazi na Serikali ya rais Weah ili kuhakikisha makabidhiano ya ofisi yanafanyika kwa utulivu.
“Nyinyi watu wa Liberia mumezungumza, mumweka imani yenu kwangu ya kuongoza mabadiliko ambayo mnataka na mabadiliko hayo yanaanza sasa hivi.” alisema Joseph Boakai.
Makamu huyo wa zamani wa rais, alitangazwa mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi wa urais baada ya kupata kura asilimia 50.64 ya kura zote dhidi ya rais anayeondoka madarakani George Weah.
Boakai anatarajiwa kushika hatamu ya kuongoza taifa hilo mwezi Januari baada ya muda wake Weah kukamilika.
Katika hotuba yake aliyoitoa katika afisi yake ya kibnafsi katika jiji kuu la Monrovia, Boakai pia aliwashukuru raia wa Liberia kwa kumchagua.