Raia nchini Liberia wanapiga kura kuwachagua viongozi wao wapya, uchaguzi ambao rais wa sasa George Weah, anawania kuongoza taifa hilo kwa muhula wa pili.
Wapiga kura kwenye taifa hilo watapiga kura kuwachagua viongozi wapya baada ya tume ya uchaguzi nchini humo kutangaza kumalizika kwa kampeni siku ya Jumapili.
Zaidi ya wapiga kura milioni mbili wameidhinishwa kushiriki uchaguzi huo ambao rais wa sasa George Weah anakabiliwa na upinzani kutoka kwa wagombea wengine 19.
Makamu wa rais wa zamani Joseph Boakai na mfanyibiashara Alexander Cummings wametajwa kuwa wapinzani wakuu wa rais Weah.
Kuelekea uchaguzi huo, tume ya ECOWAS imewataka wanaogombea kuepuka kuzungumzia mambo yanayoweza kuzua wasiwasi na machafuko.
Hali ya wasiwasi ilishuhudiwa wakati wa kipindi cha kampeni, vurugu zikishuhudiwa katika jimbo la Lofa kati wa wafuasi wa rais anayeondoka madarakani na wafuasi wa upinzani.
Weah aliingia mdarakani mwaka wa 2017 baada ya majaribio mawili ya hapo awali kutofanikiwa.