Mahakama ya Rufaa katika mji wa al Bayda, umbali wa kilomita 800 mashariki mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli imewahukumu watu hao 37 wenye mfungamano na genge la uhalifu lililoratibu safari ya wahajiri 11 walioaga dunia baharini wakisafirishwa kwa boti iliyochakaa.
Mahakama nchini Libya imeidhinisha hukumu kali kwa watu 37 waliotuhumiwa kujihusisha na magendo ya binadamu.
Watu hao wanatajwa kusababisha vifo vya wahajiri waliokuwa wakijaribu kuelekea Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania. Haya yameelezwa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Libya.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama hiyo ya Rufaa ya Libya ambayo haikutaja uraia wa watuhumiwa hao, imesema kuwa watu 37 wamepatikana na hatia; 5 miongoni mwao wakiwa wamehukumiwa kifungo cha maisha jela, 9 kifungo cha miaka 15, na waliosalia kifungo cha mwaka mmoja jela.
Katika ripoti iliyochapishwa mwezi Machi, ujumbe wa kutafuta ukweli wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Libya ulidai kuwa wahamiaji walionaswa nchini Libya walipunguzwa utumwa wa ngono, uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Kundi hili la wataalam tayari lilikuwa limetaja uhalifu dhidi ya ubinadamu katika vituo vya kizuizini vya wahamiaji nchini Libya, lakini hii ilikuwa mara ya kwanza kuliangalia suala la utumwa.
Mnamo Oktoba 2021, Marekani na Umoja wa Mataifa ziliweka vikwazo kwa raia wa Libya, Osama Al Kuni Ibrahim, anayetuhumiwa kwa “unyanyasaji wa kutisha dhidi ya wahamiaji wa Kusini mwa Jangwa la Sahara” katika kituo cha kizuizini nchini Libya.