Kundi la Wanigeria 161 wamerudishwa makwao kutoka Libya kama sehemu ya mpango wa hiari unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, shirika la habari la AFP linaripoti.
Waliwasili kwa ndege kutoka Tripoli kwenye uwanja wa ndege katika jiji kuu la Lagos siku ya Jumatatu, inasema.
Walijumuisha wanawake 75 na watoto sita ambao walikuwa wamefungwa katika vituo vya kizuizini nchini Libya.
Waziri wa mambo ya ndani wa Libya alinukuliwa akisema kuwa 102 kati ya waliorejeshwa makwao wamesimamishwa kwenye mpaka kati ya Libya na Tunisia.
Libya ni njia kuu ya wahamiaji lakini mbaya kwa Waafrika wanaotaka kuvuka kwenda Ulaya kinyume cha sheria kupitia Bahari ya Mediterania.
Afisa katika ubalozi wa Nigeria nchini Libya alithibitisha kwa AFP kwamba wahamiaji hao hawakulazimika kurejea nyumbani.
“Tulizungumza nao na kueleza kuwa uhamiaji sio mbaya… lakini unapaswa kufuata utaratibu unaostahili,” mshauri wa ubalozi Samuel Okeri alinukuliwa akisema.
“Wanarudi kwa hiari. Na kama unavyoona, hawana huzuni bali wanafurahi kurudi Nigeria. Hakuna mahali kama nyumbani.”