Katika taarifa za kushangaza ambazo zimezua taharuki katika ulimwengu wa soka, ni kuhusu rais wa La Liga Javier Tebas kufichua kuwa Lionel Messi alikuwa anakaribia kurejea Barcelona kabla ya kuamua kujiunga na Inter Miami.
Tebas, akizungumza katika mahojiano yaliyoripotiwa na Kick TV kupitia The Mirror, alifichua ukaribu wa kuungana kwa Messi na klabu yake ya zamani, akisema, “Binafsi, kwa sababu ya hamu ya Messi na Barca, niliona kuwa karibu.”
Tebas alifafanua juu ya uwezekano wa mpango huo, akisisitiza uhusiano wa kihisia kati ya Messi na Barcelona ambao ulionekana kuandaa njia ya kurejea.
“Kunapokuwa na mapenzi hayo, masuala mengi ya kiuchumi huachwa kando. Niliona inawezekana niliona karibu nina hakika kwamba Messi angependa kustaafu akiwa Barca,” aliongeza, akisisitiza hisia za pande zote mbili.
Hata hivyo, uamuzi wa Messi kukwepa kurejea Catalonia ulitokana na wasiwasi uliozingira mazingira ya kutatanisha ya kuondoka kwake katika klabu hiyo.
Messi aliwahi kuzungumzia uvumi wa kutaka kustaafu Barcelona mnamo Juni 2023, Messi alieleza kwa uwazi, “Nilitaka sana, nilifurahi sana kuweza kurudi, lakini baada ya kupata uzoefu niliopitia na kuondoka niliokuwa nao [mara ya mwisho], Sikutaka kuwa katika hali ileile tena.”