Waziri wa Nishati January Makamba kwenye mazungumzo yake na Waandishi wa habari amesema kuwa Mawaziri 6 kutoka Tanzania na Zambia watakutana kwenye kikao kazi kitakachojadili ushirikiano baina ya nchi hizi mbili katika ulinzi na usalama wa Bomba la Mafuta la TAZAMA na sekta ya nishati kwa ujumla wake. Kikao kazi hiki, kitatathmini utekelezaji wa masuala ya ulinzi na usalama wa bomba la mafuta la TAZAMA ambalo tayari limeanza kazi ya kusafirisha mafuta ya Dizeli toka Dar kwenda Zambia.
Akielezea umuhimu wa kikao hicho na mrejesho wa kikao cha awali Waziri Makamba amesema>> ‘Bomba hili kwa sasa linasafirisha Lita Milioni 90 kwa mwezi kutoka hapa nchini kwenda Zambia, na tafsiri yake kama bomba hili litakua na ufansi zaidi Zambia wataendelea kuitumia Bandari ya Dar es salaam ili kuingiza mafuta nchini kwao na bandari ya Dar itapata soko zaidi kwa mafuta yanayoenda zambia na hatimae yale yanayoenda Kongo.
Waziri Makamba amesema haya ni mashirikiano mazuri kati ya nchi zetu hizi na pia ni mwendelezo wa mahusiano mema unaofanywa na Viongozi wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Hakainde Hichilema, Rais wa Jamhuri ya Zambia kama yalivyoasisiwa na Viongozi wetu wa kwanza Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere na Hayati Kenneth Kaunda.