Klabu ya Liverpool imeendelea kutuama kileleni mwa Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza (EPL) na kujiweka pazuri kutawazwa mabingwa wa kipute hicho msimu huu baada ya kuitandika Brentford wikendi mabao 4-1 katika Uwanja wa Brentford Community.
Darwin Nunez aliwafungulia Liverpool ukurasa wa mabao kunako dakika ya 35 kabla ya magoli mengine kufumwa wavuni katika kipindi cha pili kupitia kwa Alexis Mac Allister, Mohamed Salah na Cody Gakpo.
Bao la Salah lilikuwa lake la kwanza mwaka huu akivalia jezi za Liverpool.
Nyota huyo raia wa Misri alikuwa akiwajibikia Liverpool kwa mara ya kwanza tangu apate jeraha la paja mwezi uliopita akicheza dhidi ya Ghana kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Ivory Coast.