Mahakama Kuu ya Tanzania imesema Septemba 9, 2019 itatoa uamuzi wa jumla kuhusu kesi ya Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu kutetea ubunge wake wa jimbo la Singida Mashariki.
Kutokana na hatua hiyo, Mbunge mteule wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu anaweza kuapishwa muda wowote kuanzia sasa.
Hatua hiyo inatokana na Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Sirilius Matupa kupanga tarehe hiyo ya Septemba 9, huku akisema hana haraka ya kutoa uamuzi huo siku ya leo ili asiathiri uamuzi wa jumla atakaoutoa.
Jaji Matupa amesema zipo kesi za kupinga ubunge mahakamani zinaendelea, hivyo mbunge anaweza kuapishwa na kisha akatenguliwa kwa amri ya mahakama.
Kutokana na hatua hiyo amesema atatoa uamuzi wa kesi hiyo Septemba 9, 2019.
Kesi hiyo imeanza kusikilizwa saa 4 asubuhi hadi muda huu mbele ya Jaji Sirilius Matupa ambapo Lissu akiwakilishwa na Mawakili wanne huku Kiongozi wa jopo akiwa Peter Kibatala.
Katika usikilizwaji wa kesi hiyo aliyeanza kuwasilisha hoja ni Wakili Kibatala ambaye amedai hatua zilizochukuliwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kutangaza kuwa jimbo analoliongoza Lissu la Singida Mashariki lipo wazi kilifanyika bila haki ya Lissu kusikilizwa.
Kibatala amedai mchakato wa kumvua Lissu ubunge haukuwa shirikishi na kwamba hajawai kutaarifiwa rasmi sababu za yeye kutenguliwa ubunge wake bali alisikia barabarani.
“Mleta maombi hakuwahi kutaarifiwa rasmi sababu za ubunge wake kutengeuliwa alisikia barabarani tu,”
“Spika anatekeleza majukumu yake kwa kuongozwa na kanuni za Bunge, katiba pamoja na kupitia maamuzi ya Maspika waliopita, hata hivyo kanuni hizo zinamtaka kutoa uamuzi kwa kuzingatia haki bila upendeleo,” ameeleza Kibatala.
Miongoni mwa hoja za Wakili wa Serikali Mkuu, Aboubakary Gurisha amedai kuwa hati ya kiapo ina mapungufu kwani kimsingi Mleta maombi (Lissu) hajaonyesha ni kwa sababu haki zimepotea, hivyo maombi hayo hayana msingi wa Mahakama kuyasikiliza.