Rais Dr. John Magufuli amewahakikishia Mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa waliopo nchini kuwa katika mwaka 2018 Serikali yake itaendeleza juhudi za kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo mapambano dhidi ya rushwa, kuboresha miundombinu ya barabara, reli na usafiri wa anga, kuongeza uzalishaji wa umeme.
Rais Magufuli amesema hayo leo February 9, 2018 katika hafla ya mwaka mpya aliyowaandalia Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Kutokana na dhamira hiyo Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi hao kuwahamasisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nchi zao, kuja hapa nchini kuwekeza na kufanya biashara mbalimbali na kwamba Serikali itatoa ushirikiano wowote utakaohitajika.
Aidha, Rais magufuli amesema mwaka 2017 ulikuwa wenye mafanikio makubwa kwa Serikali kitaifa na kimataifa, ambapo iliendelea kutekeleza mpango wa maendeleo wa miaka 5 unaolenga kuiwezesha nchi kuwa ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na ametaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi kulikowezesha kuongezeka kwa mapato kwa asilimia 7.87.
Kuhusu azma ya kujenga viwanda, JPM amesema utekelezaji wa azma hii unakwenda vizuri ambapo katika kipindi cha miaka miwili viwanda 3,500 vimejengwa na vingine vingi vinaendelea kujengwa.
Rais Magufuli amesema kama ilivyofanya katika mwaka 2017 Tanzania itaendelea kutekeleza majukumu mbalimbali ya kikanda na kimataifa ikiwemo kushiriki katika juhudi za kutafuta amani, kushiriki harakati za usuluhishi wa migogoro ikiwemo ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jamhuri ya Afrika ya Kati, Lebanon, Sudan na Sudani kusini.
Hata hivyo JPM ameelezea kusikitishwa na uamuzi wa Umoja wa Mataifa kuanza kutekeleza sera ya kupunguza gharama kwenye misheni za kulinda amani kwani kwa kufanya hivyo itadhohofisha jitihada za kutafuta amani kwenye maeneo yenye migogoro na kuhatarisha maisha ya walinda amani pamoja na raia wasio na hatia.
Pia, Rais Magufuli amesema pamoja na nia njema ya mpango wa majaribio wa kutafuta suluhu la kudumu ya tatizo la wakimbizi Tanzania imeamua kujitoa kutokana na changamoto za kiusalama na ukosefu wa fedha za kugharamia mpango huo.
JPM amezungumzia taarifa za kukamatwa kwa meli zenye kupeperusha bendera ya Tanzania zikiwa zimehusika katika uhalifu na kuwahakikishia Mabalozi hao kuwa meli hizo sio za Tanzania bali zilijipatia usajili wa Tanzania, na kwamba kufuatia hali hiyo Tanzania imechukua hatua ya kusitisha usajili wa meli zote 470 zenye usajili wa Tanzania.
Nae Naibu Kiongozi wa Mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa hapa nchini ambaye ni Balozi wa Saharawi Brahim Salehe El-Mami Buseif amempongeza JPM na Serikali yake kwa juhudi kubwa zilizofanyika kuimarisha huduma za afya, elimu, maji na kuongeza ukusanyaji wa mapato na ameahidi kuwa Mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa wataendelea kushirikiana na Serikali katika kufanikisha miradi mbalimbali.
PETER KIBATALA AMEZUNGUMZA BAADA YA SUGU KUACHIWA, AMETAJA KILICHOKUWA KINAKWAMISHWA DHAMANA