Baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Klabu ya Singida United iliyopanda Daraja kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao Mlinda mlango Ally Mustapha ‘Barthez’ amewasili Mwanza kujiunga na timu hiyo.
Ally Mustapha alisaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Singida United moja kati ya timu tatu za Ligi Kuu zinadhaminiwa na SportPesa akitokea Yanga SC na tayari ameungana na wachezaji wenzake walioweka kambi ya mazoezi Mwanza kujiandaa na Ligi Kuu mwezi ujao.
Katibu Mkuu wa Singida United ambayo ilisaini mkataba wa udhamini wa mwaka mmoja na SportPesa mapema mwaka huu, Abdulrahman Sima alimpokea Ally Mustapha alipowasili katika mazoezi ya timu hiyo Uwanja wa Nyamagana saa 3:30 Asubuhi kabla ya kukutana na Kocha Hans van der Pluijm na wachezaji baada ya kumaliza mazoezi.
>>>”Nina furaha kujiunga na Singida United kwa sababu ni timu inayoonekana kuwa itakuja kuleta upinzani kwa Tanzania. Nina matarajio ya kufanya vizuri nikiwa na Singida United kwa sababu nakutana na mwalimu ambaye nilikuwa naye Yanga. Kwa hiyo, najua tutafanya vizuri.
“Nimeamua kutoka Yanga kuja huku ili niweze kubadilisha mazingira na nina Imani nitafanya vizuri kwa sababu kuna wachezaji tayari nawajua. Ninapenda kuwaambia mashabiki wa Singida United kuwa waiunge mkono timu yao kwa sababu timu inatakiwa kuwa na viongozi, wachezaji na mashabiki pia ambao ni wachezaji wa 12. Hivyo watuunge mkono na tukiwa pamoja tutafanya vizuri.” – Ally Mustapha.