Kutokana na kuongezeka kwa kesi zinazohusisha usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya Tanzania, serikali imeamua kuandaa mkakati mpya ambao utasaidia namna ya kupambana na tatizo hilo.
Katika taarifa iliyoripotiwa na kituo cha TBC 1, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge William Lukuvi ametoa taarifa hii “Tulinusuru taifa kwani Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.. aidha katika kukabiliana na tatizo hili la dawa za kulevya nchini, kama nilivyokuwa nimeahidi mwaka jana, Serikali imetunga tayari sheria mpya kali zaidi itakayoondoa changamoto zilizokuwepo na zilizokuwa zinajitokeza, wakati wa matumizi ya sheria inatumika sasa, sheria ya kuzuia biashara haramu ya dawa za kulevya namba tisa ya mwaka 1995..”– Lukuvi.
“..Muswada huu wa sheria ni mpya unaitwa muswada mpya ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, utawasilishwa bungeni na kusomwa mara ya kwanza katika mkutano huu wa Novemba, lengo ni kwamba mswada huu ukishawasilishwa uwe ni wazi kwa wananchi wote kutoa maoni, kamati za bunge kuanza kujadili hili ifikapo katika bunge la mapema mwakani uweze kupitishwa na kuwa sheria kali itakayotumika na kuunda chombo kipya kitakachukua na nguvu zaidi ukilinganisha na hali ilivyo hivi sasa..”– Lukuvi.
Pamoja na kutunga sheria kali Waziri Lukuvi ameelezea mafanikio yaliyopatikana licha changamoto zilizopo; “..Hali hii inaonyesha na ongezeko la jitihada za kukabiliana na uzalishaji wa dawa za kulevya nchini, pamoja na uwepo wa tatizo la matumizi na biashara za dawa za kulevya, nchi yetu inatuhumiwa kupitisha malighafi za kuzalishia dawa za kulevya mwaka 2013 tofauti na miaka ya nyuma, napenda kuwapongeza watendaji wetu wa taasisi ya udhibiti na wadau wote na Task Force waliojitoa kimasomaso kuleta mafanikio haya..”
“..Niwakumbushe wananchi kuwa matumizi na biashara za dawa za kulevya yanaleta madhara makubwa kwa taifa letu, kiafya, kijamii , kiuchumi, kiusalama na kimazingira, hivyo nawaomba sana wananchi mtoe taarifa kwa vyombo vya dola kuhusu biashara za dawa za kulevya hii ikiwa ni pamoja na kilimo cha bangi katika maeneo yenu..”– Lukuvi.
Kuisikiliza taarifa ya kituo cha TBC 1 unaweza kubonyeza play hapa.