Watabiri wa hali ya hewa huko California Nchini Marekani wametoa tahadhari juu ya upepo mkali ambao ulisababisha moto Los Angeles unatarajiwa kushika kasi tena wiki hii, huku vikosi vya zima moto wakiendelea na jitihada za kudhibiti mioto hiyo mitatu ya nyikani.
Maafisa wa eneo hilo walionya kuwa baada ya juma la upepo uliopungua kasi kiasi, upepo uliokauka wa Santa Ana utavuma tena kuanzia Jumapili usiku hadi Jumatano, na kufikia kasi ya hadi 60mph (96km/h).
Kabla ya kurejea tena kwa upepo huo, kuna hatua ambazo zimefikiwa kuzuia kuenea kwa mioto mikali ya Palisades na Eaton, ambayo inawaka pande tofauti za jiji.
Wazima moto wa eneo hilo wanasaidiwa na wafanyakazi kutoka majimbo mengine manane ambayo ni pamoja na Canada na Mexico, ambao wanaendelea kuwasili.
Mchunguzi wa afya wa Kaunti ya L. A alitoa taarifa za idadi ya waliofariki hadi Jumapili kufikia 24.
Awali, maafisa walisema takriban wengine 16 hawajulikani walipo huku Kumi na sita kati ya waliofariki walipatikana katika eneo la moto la Eaton, huku wanane wakipatikana katika eneo la Palisades.
Moto mkubwa zaidi ni Palisades, ambao sasa umeteketeza zaidi ya ekari 23,000 na kudhibitiwa kwa 11%.
Moto wa Eaton ni wa pili kwa ukubwa na umeteketeza zaidi ya ekari 14,000. Umedhibitiwa kwa asilimia 27.
Moto wa tatu wa Hurst umeenea hadi ekari 799 na karibu unadhibitiwa wote kabisa.
Siku ya jana Jumapili, wazima moto waliweza kuzuia haraka kuenea kwa moto uliokuwa unaanza kuwaka katika Msitu wa Kitaifa wa Angeles, unaozunguka eneo ambalo ni kitovu cha mpango wa anga za juu wa Marekani na una teknolojia ya siri ya juu.