Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ameshinda kura za kwanza za mchujo zaa chama cha Republican katika jimbo la Iowa Jumatatu jioni, kulingana na makadirio ya vyombo vya habari vya Marekani. Anajumuisha hadhi yake ya kupewa nafasi kubwa ya ushindi kwa mrengo wa kulia kwa uchaguzi wa urais mnamo Novemba.
Donald Trump ameshinda kura za mchujo za chama cha Republican katika jimbo la Iowa Jumatatu jioni, vyombo vya habari vya Marekani vimetangaza takriban nusu saa baada ya kuanza kwa kura hiyo.
Kulingana na kituo cha televiseni cha CNN, bilionea huyo mwenye umri wa miaka 77, aliyeshtakiwa mara nne kwa uhalifu, anaongoza kwa kura nyingi dhidi ya wapinzani wake wakuu Nikki Haley na Ron DeSantis, hata kama matokeo bado ni ya muda.
Uchaguzi huu wa kura za mchujo huko Iowa unachukuliwa kuwa muhimu zaidi, kwa sababu jimbo hili ndilo la kwanza kupiga kura: kwa hivyo kura hizi zinatoa nafasi kwa mchakato mzima wa uchaguzi unaoendelea hadi mwezi Juni, na kwa hili, wagombea wanazingatia juhudi zao zote za kampeni katika jimbo hili dogo la vijijini la Kati Magharibi lenye watu takriban milioni tatu.