Manchester United itakosa beki wa kushoto anayetambulika baada ya klabu hiyo kuthibitisha kwamba Luke Shaw atakosa “miezi michache” ya msimu huu.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza pia atakosa mechi za kirafiki za Three Lions dhidi ya Brazil na Ubelgiji mwezi ujao, huku Gareth Southgate akitoa jasho kuhusu utimamu wa beki huyo kuelekea michuano ya Euro 2024, itakayoanza kwa Uingereza Juni 16 dhidi ya Serbia.
Manchester United imethibitisha kuwa Luke Shaw atakuwa nje kwa “miezi michache” kutokana na jeraha, na kumwacha Erik ten Hag bila beki wa kushoto anayetambulika.
Shaw alitolewa nje katika mechi zote mbili zilizopita za United – wakati wa mapumziko dhidi ya Aston Villa, na katika kipindi cha kwanza katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Luton – huku Ten Hag akisema kwamba maamuzi yake yalikuwa ya tahadhari.
United ilithibitisha habari hizo kwenye tovuti rasmi ya klabu, ikisema: “Tathmini zaidi bado inahitajika kubaini ukali lakini tunatarajia kuwa hayupo kwa miezi michache.”