Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kuwakamata raia wanne wa Msumbiji na mmoja wa Afrika Kusini, Phila Tshabalala wanaodaiwa kumteka nyara Mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji maarufu MO.
Mshtakiwa mmoja ambaye ni dereva taksi na Mkazi wa Tegeta, Mousa Twaleb (46) tayari alishafikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Hakimu Shaidi alitoa hati ya kuwakamata washitakiwa hao ambao wengine ni Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issac Tomo na Zacarious Junior wote raia wa Msumbiji.
Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon kudai kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na hivyo wanaomba hati ya kuwakamata washitakiwa hao.
Simon alidai washitakiwa hao wataunganishwa katika kesi hiyo kujibu mashitaka mawili ya kumteka nyara MO kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari na kuongoza genge la uhalifu.
Inadaiwa Mei Mosi, 2018 na Oktoba 10, mwaka huo huo, katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam na Johannesburg Afrika Kusini, kwa makusudi washitakiwa wote kwa pamoja waliendesha genge la uhalifu.
Pia inadaiwa Oktoba 11, mwaka jana maeneo Hoteli ya Colloseum wilayani Kinondoni Dar es Salaam, Twaleb pamoja na watu wengine ambao hawapo mahakamani, walimteka nyara MO kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.
Pia inadaiwa Julai 10, mwaka jana maeneo ya Mbezi Beach wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Twaleb alitakatisha fedha ambazo ni Sh 8,000,000 wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.
MO alitekwa nyara Oktoba 11, mwaka jana alfajiri maeneo ya Hoteli ya Colloseum wakati akienda kufanya mazoezi na alipatikana Oktoba 20, mwaka huo huo katika eneo la Gymkhana.