Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuhukumu kwenda jela mwaka mmoja, Mchungaji Kanisa la The Hill Lord, David Chirhuza (33) na wake zake wawili kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.
Pia mahakama imemuhukumu Mchungaji huyo mwenye wake watatu na watoto sita, kwenda jela mwaka mmoja kwa kufanya kazi ya uchungaji bila kibali cha makazi.
Hatua hiyo inatokana na mahakama hiyo kumtia hatiani Mchungaji na wake zake wawili na mdogo wake baada ya kukiri makosa ya kuingia nchini bila kibali akitokea nchi ya Congo DRC.
Pia kukiri kosa la kufanya kazi ya uchungaji bila kibali cha makazi kabla ya kuahirishwa kwa muda na kutoa adhabu hiyo.
Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustino Mmbando baada ya washitakiwa kusomewa mashtaka yao na kukiri.
Mbali na mchungaji washtakiwa wengine ni Esther Sebuyange (27), na Kendewa Ruth (26) (wake wa Mchungaji) na Mshtakiwa mwingine mdogo wa Mchungaji, Samuel Samy (22).
Baada ya kusomewa mashtaka yao, Mchungaji David alikiri shtaka la kwanza la kuingia nchini bila kibali na kukiri shtaka la pili kufanya kazi ya uchungaji huku akiwa hana kibali cha makazi.
Washtakiwa wengine walikiri shtaka la kuingia nchini bila kibali
Washtakiwa hao kabla ya kuhukumiwa waliomba mahakama iwasamehe, isiwape adhabu kali, huku Mchungaji akisema kazi alivyokuwa akiifanya ya kuhudumia jamii si biashara pia kusimamia sheria ya Mungu.
Mashitaka waliyosomewa inadaiwa kwamba, Septemba 2 mwaka huu eneo la Salasala Kilimahewa, Dar es Salaam, mchungaji huyo na wenzake walibainika kuingia nchini bila kibali.
Katika shtaka la pili, ilidaiwa mchungaji huyo pekee alibainika kujihusisha na kazi za kanisa akiwa hana kibali cha makazi.