Tume ya Ushindani nchini, FCC, imezindua Maadhimisho ya Wiki ya Ushindani Duniani ikiwa na lengo la kuelimisha wadau mbalimbali wakiwemo Wachimbaji Wadogo wa Madini pamoja na Wakulima wa Korosho juu ya athari za upangaji njama hususani katika bei za bidhaa unavyoweza kufifisha ushindani katika soko.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa FCC William Erio, amesema Wiki ya Ushindani inayoanza Novemba 30, hadi Desemba 05, 2023, itatumika kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiasha na wenye viwanda kutoa semina zenye zinazolenga kuwakumbusha kufuata Sheria na Kanuni zinazosimamia masuala ya ushindani wa biashara nchini huku siku ya kilele cha maadhimisho hayo Desemba 5, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt Ashatu Kijaji ambapo Kauli Mbiu ya Maadhimisho hayo ni NJAMA BAINA YA WASHINDANI NA MADHARA YAKE KWA WALAJI NA WATUMIAJI
Mkurugenzi Mkuu huyo amesema,Tume ya Ushindani pia itaenda katika baadhi ya Mikoa kukutana na wadau ana kwa ana hususan wafanyabiashara ili kuongeza uelewa wa kutambua viashiria vya uwepo wa bidhaa bandia na athari zake kiuchumi na kwa mlaji.