Nchini Kenya, polisi wanne wamewakamata baada ya maafisa wa upelelezi kutekeleza oparesheni kwenye nyumba ambako raia wa Ethiopia 37 walikuwa wanazuiliwa, kilomita 16 kutoka mji mkuu, Nairobi.
Maafisa hao wanadaiwa kuhusika na biashara ya ulanguzi wa binadamu.
Kwa mujibu wa gazeti la ndani la The Star, raia hao wa Ethiopia waliambia mamlaka ya Kenya kwamba walikuwa wakielekea Afrika Kusini kutafuta maisha bora.
Msako unaendelea kumtafuta mwenye nyumba hiyo na washiriki wake wengine wa mtandao wa ulanguzi wa binadamu.
Wahamiaji wa Ethiopia wamekuwa wakitumia njia ya Kenya wakati wakijaribu kuvuka kuingia Afrika Kusini kinyume cha sheria, kwa mujibu wa taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM.
IOM inaeeleza kuwa wahamiaji hao, ambao wengi wao ni wanaume kutoka mikoa ya Oromia na SNNP nchini Ethiopia wanaingia Kenya kupitia mpaka wa Moyale, kabla ya kuelekea Tanzania na hatimaye Afrika Kusini.