Takriban maafisa wanane wakuu katika Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa nchini Kenya (KeBS) wamesimamishwa kazi kutokana na sakata la mbolea feki.
Uchunguzi unaendelea kuhusu suala hilo unaofanywa na Ofisi ya idara ya upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) na Bunge.
Maafisa walisema wanane hao walizuiliwa kutokana na utoaji wa vyeti na nembo za ubora wa bidhaa kwa kampuni mbili, ambazo zimehusishwa na mbolea ya kiwango cha chini.
Wanane hao walikuwa miongoni mwa waliohojiwa na DCI siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.
Maafisa wa upelelezi wamewataka maafisa kadhaa wa mashirika ya serikali ambao walishughulikia mbolea hiyo bandia ambayo inaendelea kuuzwa kufika katika ofisi zao.
Maafisa walisema wamewaita wale wote wanaohusika na upatikanaji na usambazaji wa mbolea hiyo ‘feki’.
Timu hiyo imepanga kulifikisha suala hilo katika ngazi yoyote kabla ya kupeleka faili lao kwa Mkurugenzi wa Mashtaka na mapendekezo mbalimbali.