Maafisa wa Taliban wanawapeleka wanawake wa Afghanistan gerezani ili kuwalinda dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa Alhamisi.
Kabla ya kundi la Taliban kunyakua mamlaka mwaka 2021, kulikuwa na vituo 23 vya ulinzi vya wanawake vilivyofadhiliwa na serikali nchini Afghanistan ambapo manusura wa unyanyasaji wa kijinsia wangeweza kutafuta hifadhi. Sasa hakuna, ripoti ya Umoja wa Mataifa ilisema.
Maafisa wa utawala unaoongozwa na Taliban waliuambia Ujumbe wa Usaidizi wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan kwamba hakuna haja ya makazi kama hayo au kwamba ni dhana ya Magharibi.
Taliban huwapeleka wanawake gerezani ikiwa hawana jamaa wa kiume wa kukaa nao au ikiwa jamaa wa kiume wanachukuliwa kuwa sio salama, ripoti hiyo ilisema.
Wanawake wanapelekwa gerezani kwa ajili ya ulinzi wao “sawa na jinsi magereza yametumiwa kuwahifadhi waraibu wa dawa za kulevya na watu wasio na makazi huko Kabul,” ripoti hiyo ilisema.
Shirika la Habari la Associated Press liliwasiliana na wizara zinazoongozwa na Taliban kuhusu ni wapi walionusurika katika unyanyasaji wa kijinsia wanaweza kutafuta usaidizi, ni hatua gani za ulinzi zimewekwa, na viwango vya kutiwa hatiani kwa wakosaji, lakini hakuna aliyepatikana kutoa maoni.
Wanawake na wasichana wamekuwa wakizuiliwa majumbani mwao zaidi tangu kutwaliwa kwa Taliban mwaka wa 2021.
Wanazuiwa kupata elimu zaidi ya darasa la sita, ikiwa ni pamoja na chuo kikuu, maeneo ya umma kama vile bustani, na kazi nyingi.