Waziri wa Nishati January Makamba amewaelekeza viongozi na wafanyakazi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuongeza nguvu katika aina nyingine za nishati kama inavyofanyika kwenye umeme.
Amesema kuwa REA imeendelea kutekeleza kwa ufanisi mkubwa usambazaji nishati ya umeme vijijini hivyo ni vyema pia ikifanya hivyo katika aina nyingine za nishati zenye matumizi makubwa zaidi, hususan zinazotumika katika kupikia.
Waziri Makamba alikuwa akizungumza na wafanyakazi wa REA ili kutoa dira na mwelekeo wa Wizara ya Nishati, ikiwa ni mara ya kwanza kukutana nao rasmi tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo, takribani siku 100 zilizopita. Alizungumza na wafanyakazi hao jijini Dodoma, Desemba 20 mwaka huu.
Alisema kuwa wengi wanaitafsiri REA kuhusika na nishati ya umeme pekee kutokana na kuweka nguvu nyingi kwenye nishati hiyo, hivyo akasema ni muhimu kwa Wakala hiyo kuzipa uzito unaostahili nishati nyinginezo ambazo ni jukumu lake pia.
“Kazi ya REA ni kubwa zaidi, siyo umeme tu. Mnafanya kazi nzuri sana kwa upande wa umeme hivyo toeni uzito unaostahili kwa nishati nyingine zenye matumizi makubwa.”
Akitoa mfano, Waziri Makamba alieleza kuwa tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa kwa Tanzania, matumizi makubwa ya nishati yako majumbani. Aidha, aliongeza kuwa nishati inayotumika zaidi majumbani hususan katika kupikia ni tungamotaka.
Alisema, asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi vijijini na wanatumia nishati ya tungamotaka katika kupikia. “Nataka mfanye mabadiliko kwenye nishati ya kupikia maana ndiyo inagusa Watanzania wengi zaidi,” alisisitiza Waziri.
Akifafanua, alieleza kuwa pamoja na kupeleka umeme vijijini, haitegemewi kuwa wakazi wake watatumia nishati hiyo kupikia hivyo ni jukumu la Wakala kufanyia kazi suala hilo.
Sambamba na agizo hilo, Waziri Makamba aliitaka REA kuimarisha Kitengo chake cha Utafiti na kianze mara moja kufanya tafiti mbalimbali zitakazoleta mapinduzi makubwa katika sekta ya nishati, hususan vijijini.
“Mathalani, kuna mawazo au fikra gani mpya kuwasaidia Watanzania wapate nishati safi ya kupikia? Je, nishati ya kupikia ina mchango gani katika kuongeza au kupunguza gharama za maisha? Hizi ni baadhi ya tafiti zinazopaswa kufanyika,” alisisitiza Waziri.
Katika hatua nyingine, Kiongozi huyo mwenye dhamana na sekta ya nishati nchini, alitoa maagizo kuwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini, wanapobainika kufanya udanganyifu kwenye miradi hiyo, wachukuliwe hatua kali ikiwemo kuondolewa kabisa na wasipewe tena fursa ya kufanya kazi hizo.
Vilevile, washitakiwe kwa Mamlaka zote husika pamoja na kufanya ufuatiliaji ili wasipewe kazi nyingine katika eneo lolote ili iwe fundisho kwao kwa kuwaumiza wananchi na kuliingizia hasara Taifa.
Pamoja na maelekezo hayo, Waziri aliipongeza REA kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanya na kuitaka kuongeza juhudi zaidi katika kuwatumikia Watanzania.
Alisema kuwa Serikali inajivunia utendaji kazi wa REA na kwamba ni mojawapo ya Taasisi zinazotegemewa sana hivyo akaiasa isiharibu sifa hiyo.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu kwa Waziri, alieleza kuwa kazi kubwa imefanyika ambapo hadi sasa upatikanaji umeme vijijini umefikia asilimia 69.6.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo, akizungumza kwa niaba ya Bodi, alimuhakikishia Waziri kuwa maelekezo yote aliyoyatoa yatafanyiwa kazi.
Waziri aliahidi kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa REA ikiwemo upandishwaji madaraja na kukaimu nafasi mbalimbali kwa muda mrefu, kama alivyowasilisha Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi, Tawi la REA, Swalehe Kibwana.