Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Bw. Onesmo Olengurumwa amaliza ziara yake kwa kanda ya pwani ya kusini kwa mikoa ya Lindi, Mtwara, na Ruvuma.
Ziara hii iliyoambatana na usaidizi wa karibu kutoka kwa Mratibu wa Kanda ya Pwani ya Kusini, Bw. Clemence Mwombeki, ilikua ni ziara ya takribani siku saba za kutembelea mashirika zaidi ya 20 katika mikoa ya kanda ya pwani ya kusini na mikoa ya karibu (Njombe na Iringa).
Katika ziara hii, wanachama wa Mtandao walifurahi sana kupokea ugeni kutoka Mratibu Kitaifa, Mratibu wa Kanda hiyo, na Afisa Dawati la Wanachama. Ziara ilitumika kama nafasi ya secretariat ya Mtandao kudumisha mahusiano na mashirikiano na wanachama wake, pamoja na;
• Mtandao kufahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili wanachama wa kanda hiyo
• Kuunda mikakati kadhaa ya kuwastawisha wanachama wake wa kanda hiyo
• Mtandao kujifunza maeneo ya kuboresha katika mashirikiano yake na wanachama wa kanda hiyo.
Wanachama wa Mtandao wa Kanda ya pwani ya kusini wamesifika kua na mahusiano mazuri sana na mamlaka husika katika maeneo yao ya kazi, pamoja na polisi, ustawi wa jamii, na hata mashirika mengine. Hii imewasaidia kutekeleza majukumu yao na kuifikia jamii husika kwa urahisi Zaidi.
Mashirika yamefanikiwa kuendesha programu mbali mbali za utoaji elimu kwa jamii na huduma za msaada wa sheria kwa mtu mmoja mmoja kupitia wasaidizi wa kisheria (Legal Aid Providers) katika masuala ya Elimu ya Sheria pamoja na elimu kupitia vipindi vya radio na kuwafikia jamii na kuelimisha.
Mashirika yamefanikiwa kufahamika vyema kwa Jamii, Wadau wa maendeleo, mamlaka mbali mabli zikiwemo jeshi la polisi, wakuu wa wilaya, viongozi wa mila na vijiji, madawati ya jinsia pamoja na kukua na Kuwa na uwezo wa kufanya kazi za kuhudumia jamii kwa mujibu wa Katiba ya zake.
Kati ya maadhimisho mengi yaliyojadiliwa, moja ni kustawisha zaidi ofisi ya uratibu wa kanda ya pwani ya kusini ambayo ni Door of Hope to Women and Youth in Tanzania (DHWYT). Hii itasaidia utetezi wa haki za binadamu kwa ukaribu zaidi kwa kanda hiyo.
Pamoja na mafanikio makubwa ya mtandao kwa wanachama wake bado changamoto kadhaa zimekuwa zikiwakumba wanachama wa mtandao ikiwemo;
1) Changamoto za kifedha, kwani kutokana na maswala ya UVIKO 19, ambapo fedha nyingi zinazotolewa na wahisani huelekea katika miradi mingine ya kupambana na janga la CORONA kubadili uelekeo.
2) Taasisi nyingi kutokuwa na ofisi yenye nafasi kubwa ya kutosheleza wafanyakazi wote kwa shughuli za kitaasisi.
3) Kutokuwa na miradi endelevu inayoweza kusaidia mashirika kufanya shughuli kwa Muda mrefu, na kuweza kuisaidia jamii na matokeo yake kunakuwa na miradi ya muda mfupi ambayo haitatui matatizo kwa kiasi kinachotakiwa.
4) Ugumu katika upatikanaji wa ‘charitable Status’ ambao ungeziwezesha taasisi kupata msamaha wa kodi mbali mbali na kuweza kujiendesha.
5) Kwa mashirika yanayotetea haki za Watoto wa kike, changamoto kubwa imekuwa Utoroshwaji wa watoto ambao hufanywa na wazazi pindi watoto wanaporudi nyumbani kwa likizo na kuozeshwa kwa lengo la kujipatia mali. Mfano shule ya NAMNYAKI inayosimamiwa na shirika la NAMGWO imekiri kukubana Zaidi na changamoto hiyo.
Pamoja na changamoto hizo bado watetezi wa haki za binadamu kanda hii ya Pwani ya kusini wameendelea na kazi za utetezi wa haki za binadamu bila kuchoka, huku wakishirikiana na serikali kuhakikisha wananchi wa ukanda huu wanapata huduma inavyostahili.
Moja kati ya mikakati ya pamoja iliyoundwa ili kuimarisha AZAKI za kanda ya pwani ya kusini ni pamoja na uundwaji wa ofisi ya uratibu wa kanda ya Mtandao chini ya shirika la Door of Hope. Hii ni mkakati ambao utawezesha kuzidi kuunganisha nguvu ya utetezi wa haki za binadamu kwa mikoa ya kanda ya pwani ya kusini na mikoa iliyo karibu.