Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka Wakuu wapya wa Wilaya walioapishwa kuhakikisha kunakuwepo ulinzi na usalama wa kutosha katika Wilaya zao.
Dk. Mwinyi ametoa maelekezo hayo wakati alipowaapisha Wakuu wa Wilaya kumi (10) za Unguja na Pemba, katika hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Zanzibar.
Disemba 28, mwaka 2020 Rais Dk. Mwinyi alifanya mabadiliko ya Uteuzi wa Wakuu wa Wilaya 11 za Zanzibar kwa kumteua Marina Joel Thomas kuwa Mkuu wa Wilaya Kati Unguja, Issa Juma Ali (Mkoani), Hamida Mussa Khamis (Magharibi ‘B’) na CDR Mohamed Mussa Seif kuwa Mkuu wa Wilaya Micheweni Pemba.
Wengine walioteuliwa na kuapishwa ni Rashid Simai Msaraka (Mjini Unguja), Sadifa Juma Khamis (Kaskazini ‘A’), Aboud Hassan Mwinyi (Kaskazini ‘B’), Rashid Makame Shamsi (Kusini Unguja), Mgeni Khatibu Yahya (Wete) na Abdalla Rashid Ali Wilaya ya Chakechake Pemba.
Amesema viongozi hao wakiwa Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama katika Wilaya zao, wana wajibu wa kuhakikisha kunakuwepo Ulinzi na Usalama wa kutosha wakati huu ambapo matukio mbali mbali ya uhalifu yakiwa yameshamiri.
Alieleza kuwa nchi haiwezi kupata maendeleo yoyote endapo hakutakuwepo na amani na usalama na kubainisha kuwepo kwa matukio mengi ya uhalifu, ikiwemo wizi wa mazao pamoja na mifugo, kiasi ambacho baadhi ya wananchi wameamua kuachana na kilimo au ufugaji.