Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob ‘Boni Yai’ ataendelea kusalia Mahabusu baada ya leo September 23, 2024 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kushindwa kutoa uamuzi wa pingamizi la dhamana dhidi yake.
Kesi hiyo ilipangwa kutolewa uamuzi leo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga lakini ameahirisha kesi hiyo hadi September 26,2024 kutokana na Mshtakiwa kushindwa kufikishwa Mahakamani huku sababu ya kutofikishwa ikiwa bado haijajulikana.
Jacob ambaye ni Kada wa CHADEMA anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni ya kuchapishaji taarifa za uongo kwenye mitandao, kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mtandao.
Itakumbukwa September 19, 2024 Jacob alipandishwa kizimbani na baada ya kusomewa mashtaka kufuatia Jopo la Mawakili wa Jamhuri kuwasilisha hoja ya kutaka anyimwe dhamana ili kulinda usalama wake pamoja na kutaka Mahakama itoe amri kwa Mshtakiwa huyo kukubali kutoa Nywila (Password) zake za mtandao wa X (zamani Twitter).