Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mabadiliko ya tabia nchi yameleta tishio kwa afya kutokana na ongezeko la majanga ya hali ya hewa, na joto la kupindukia.
Hayo yamo katika ripoti ya kila mwaka ya hali ya hewa iliyotolewa na, Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa WM ambalo sasa linataka kuwepo kwa mifumo bora ya kutoa tahadhari inayoweza kujumuishwa katika sera ya afya ya umma.
WMO inasema taarifa kuhusiana na hali ya hewa hazijumuishwi kikamilifu katika mipango ya huduma ya afya.
Hali mbaya ya hewa inasababisha pia maradhi kwa watoto na hata wazee kutokana na ongezeko la joto ama baridi kali.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linasema joto la kupindukia ni chanzo kikubwa cha vifo vinavyotokana na hali mbaya ya hewa, ila katika nchi zilizoathirika na kadhia hiyo, ni nusu tu ya wanaofanya maamuzi kuhusiana na masuala ya afya ndio wenye uwezo wa kupata huduma za tahadhari.
Kati ya mwaka 2000 na 2019 vifo vilivyosababishwa na joto vinakadiriwa vilikuwa 489,000 kwa mwaka.
Inaelezwa kuwa, mwaka 2022, ukame, mafuriko na mawimbi ya joto yameathiri kila bara na kugharimu hasara ya mabilioni ya dola.