Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imesema imepokea taarifa na pia kuthibitisha uwepo wa baadhi ya watoa huduma wa mabasi yanayokwenda Mikoani kucheza na mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi na kusababisha kusafiri kwa mwendokasi kwa lengo la kufanya mashindano ya kufika wa kwanza kwenye vituo/stendi za mabasi hivyo imefuta ratiba za mabasi 9 yaendayo Mikoani yanayoanza safari saa 9 alfajiri.
“Watoa huduma hao wanatumia pia fursa iliyotolewa ya kuanza safari mapema (saa 9 – saa 11 alfajiri) na kufanikisha azma ya kufanya mashindano na kufika wa kwanza kwenye vituo, takribani wiki mbili sasa, kumekuwa na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha mabasi ya Ally’s Star, Katarama Express na Ismamilo yakishindana kufika katika vituo vya mabasi, basi lililoshinda lilimwagiwa maji na kushangiliwa”
“Hapana shaka na waliobashiri litawahi walipata ushindi kwenye Kamari waliyoicheza kinyume na taratibu, LATRA kwa kuzingatia jukumu lake la kukuza usalama wa sekta zinazodhibitiwa ikiwa ni pamoja na usalama wa watumiaji wa huduma za sekta zinazodhibitiwa haiwezi kuacha matendo haya hatari yenye kuhatarisha usalama na maisha ya wat pamoja na mali zichezewa bila kuchukua hatua”
“Hivyo, kutokana na hali hii na kwakuwa watoa huduma Ally’s Star na Katarama Express wameendelea kukiuka Sheria, kanuni na taratibu hata baada ya kupatiwa elimu na maonyo kadhaa, kwa kuzingatia mamlaka tuliyonayo, tumefuta ratiba zote za mabasi tisa yanayoanza safari zao kuanzia saa 9.00 alfajiri, mabasi hayo ni sita ya Ally’s Star (T946 EBF, T947 EBF, T948 EBF, T354 DXS, T357 DXS a T360 DXS) na matatu (3) na Katarama Express (T835 EBR, T836 EBR, T212 ECR), mabasi hayo sasa yatapaswa kuanza safari saa 12.00 asubuhi kuanzia Jumatano, tarehe 21 Juni, 2023, endapo wataendelea kukiuka maelekezo haya, tutafuta leseni zao”