Mabinti balehe na Wanawake Vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 Mkoani Iringa kunufaika na Mafunzo mbalimbali yanayotolewa na Mradi wa Epic unaotekelezwa na Shirika la Family Health International (FHI360) Kwa ufadhili wa mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).
Akisoma taarifa ya utekelezaji Kata ya Gangilonga, Manispaa ya Iringa katika halfa ya ufunguzi wa Kituo Cha Mafunzo ya Ufundi stadi Kwa Mabinti, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Credianus Mgimba amesema mradi wa Epic umefanikiwa kuanzisha jumla ya Vikundi 196 vya kuweka na kukopa vyenye jumla ya Mabinti 3284 ambao wamepata fursa ya kuanzisha biashara ya uzalishaji mali.
“Mradi umefanikiwa kuanzisha jumla ya vikundi 196 (60 Iringa MC, 136 Mufindi DC) vya kuweka na kukopa vyenye jumla ya mabinti 3284 (932 Iringa MC, 2352 Mufindi DC) kutoka kata mbalimbali
Mabinti hao wameweza kuanzisha biashara za mtu mmoja mmoja na wengine za vikundi biashara hizo ni kama ufugaji, magenge ya kuuza bidhaa mchanganyiko za nyumbani, maduka ya nafaka, kusindika matunda na kutengeneza jam, saloon, sabuni za maji, ushonaji wa vikapu, na mikoba” amesema Mgimba
Akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa Katibu tawala msaidizi wa Mkoa wa Iringa Venance Ntiyalundura mara baada ya Uzinduzi wa Kituo hicho Cha Mafunzo ametoa rai Kwa Viongozi wa Manispaa kuhakikisha vikundi hivyo vinapata Usajili wa Serikali vinapewa Elimu ya kitaalamu pamoja na kupewa mikopo ya Serikali ya asilimia kumi.
Aidha Ntiyalundura ameongeza Kwa kusema kuwa Serikali itaendelea kutoa Ushirikiano mkubwa kuhakikisha inaendeleza Kituo hicho hata mara baada ya kuisha Kwa mradi huo.
Vilevile Ntiyalundura amewataka mabinti hao kuwa Mabalozi wazuri Katika Jamii kwa kutoa Elimu ambayo wamepata Kwa Vijana wenzao na kuwashawishi wajiunge katika miradi yenye tija ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Nao baadhi ya Mabinti wamesema kwamba licha ya mradi huo kuwajengea uwezo wa kujiamini, kujitambua na kupima VVU na kujua hali zao za kiafya mradi huo utaenda kuleta tija kwao kwani utawasaidia kujikwamua kiuchumi.