Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amemteua Michel Barnier kama waziri mkuu karibu miezi miwili baada ya uchaguzi wa mapema Ufaransa kumalizika kwa mkwamo wa kisiasa.
Bw Barnier, 73, ndiye mpatanishi mkuu wa zamani wa Umoja wa Ulaya wa Brexit na aliongoza mazungumzo na serikali ya Uingereza kati ya 2016 na 2019.
Mwanasiasa huyo mzoefu wa chama cha mrengo wa kulia cha Republicans, amekuwa katika kisiasa kwa muda mrefu na kushikilia nyadhifa mbalimbali za juu, nchini Ufaransa na ndani ya EU.
Sasa atalazimika kuunda serikali ambayo itaepusha Bunge la Kitaifa kugawanyika katika kambi tatu kubwa za kisiasa, zisizo na uwezo wa kuunda wingi wa moja kwa moja.
Miaka mitatu iliyopita Bw Barnier alisema anataka kupambana na Rais Macron kuwa rais wa Ufaransa, akisema anataka kuweka kikomo na kudhibiti uhamiaji.
Lakini alishindwa kuchaguliwa kuwa mgombea na chama chake.
Bw Barnier anatazamiwa kuchukua nafasi ya Gabriel Attal, waziri mkuu mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuchaguliwa nchini Ufaransa, ambaye Rais Macron alimteua kwa mara ya kwanza kuwa waziri mkuu mapema mwaka 2024 na ambaye amekaa katika wadhifa wake kama kaimu tangu Julai.