Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameitangaza serikali mpya chini ya uongozi wa Francois Bayrou, Waziri Mkuu wake wa nne mwaka huu ili kuiondoa nchi hiyo kutoka kwenye mgogoro wa kisiasa.
Bayrou, mwanasiasa wa mrengo wa kati anatumai kuwa baraza lake la jipya la mawaziri linalojumuisha mawaziri wa zamani na watumishi waandamazi wa serikali litasaidia kusimamia kupitishwa kwa bajeti ya mwaka 2025 na hivyo kuondoa mkwamo ambao ulikuwa unatishia kuzidisha mzozo ndani ya nchi hiyo yenye uchumi wa pili kwa ukubwa katika Umoja wa Ulaya.
Majina ya baraza jipya la mawaziri yalisomwa na mkuu wa wafanyikazi wa ikulu Alexis Kohler.
Ufaransa imekumbwa na mkwamo tangu Macron alipocheza kamari katika uchaguzi wa ghafla msimu huu wa joto kwa matumaini ya kuimarisha mamlaka yake.
Hatua hiyo iliambulia patupu, huku wapiga kura waliokuwa wakichagua bunge kuvunjika kati ya kambi tatu zinazohasimiana.