Madaktari wa Kipalestina, Thaer Dababesh, na mchumba wake, Asma Jabr, walifanya sherehe ya harusi yao katika Hospitali ya Al-Shifa huko Gaza, ambapo wawili hao wamekuwa wakifanya kazi bega kwa bega tangu Israel ilipoanza vita vyake dhidi ya eneo lililozingirwa mwezi Oktoba, na kuua zaidi ya watu 31,000 na kujeruhi makumi ya maelfu zaidi.
Vita vilipoanza, nyumba ya wanandoa hao ililipuliwa na shambulio la anga la Israeli, na harusi yao – ambayo ilipangwa Novemba – ilibidi iahirishwe kwa muda usiojulikana.
Sasa, huku vita vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza vikiingia mwezi wa sita, wanandoa hao waliamua kufanya sherehe ya harusi katika jengo la Al-Shifa Medical Complex, magharibi mwa mji wa Gaza, miongoni mwa wenzao ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kutoa huduma za matibabu chini hali mbaya.
Sherehe rahisi ya harusi ilifanyika ndani ya hospitali, wakati ambapo bibi arusi alivaa nguo yake ya matibabu licha ya kutokuwepo kwa familia, marafiki kama sherehe za kawaida.
Familia ya bibi harusi ilifurushwa na kulazimika kuhamia mikoa ya kusini ya Ukanda wa Gaza na hawakuweza kuhudhuria sherehe ya ndoa yao.
Wanandoa hao walikuwa na matumaini kwamba wazazi na ndugu zao wangekuwepo kwenye sherehe ya harusi, pamoja na kuandaa karamu kubwa, kama ilivyozoeleka kwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, ambao unakumbwa na janga la njaa hasa kutokana na mzingiro mkali wa Israel.
Wanandoa hao hapo awali walikuwa wamefunga ndoa rasmi mnamo Julai 2023, na sherehe ya harusi yao ilipangwa Novemba 15 mwaka jana, lakini kuendelea kwa vita kulizuia hilo.