Madereva wawili wa mabasi ya Mikoani ambayo yalikuwa yanatoka Mbeya kwenda Dar es salaam ambayo ni New Force lenye namba za usajili T850 DHA pamoja na Abood lenye namba za usajili T872 DJP, wamekamatwa Mkoani Iringa wakiwa wanashindana na kuoneshana ufundi wa kuendesha kwa kasi barabarani huku wakiwa na abiria kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Madereva hao ambao ni Hashim Jumanne Fonga wa New Force na Reniely Julius wa Abood wamekamatwa leo na Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani kikiongozwa na RTO wa Iringa, Mosi Ndozero.
Akiongea na @AyoTV_ RPC wa Iringa Allan Bukumbi amesema magari hayo yalikuwa yanatoka yote sehemu moja huku yakiwa kasi bila kuzingatia sheria zozote za usalama barabarani wakiwa na abiria na amesema Madareva hao watachukuliwa hatua.
“Haya mabasi yalikuwa yanatokea sehemu moja basi la Abood lilikuwa mbele na lilikuwa linataka kulipita lori na wakati huo basi la New Force likawa linataka pia kulipita basi la Abood ambalo lilikuwa lina-ovetake lori na kumbuka mabasi haya yote yana abiria, tutawachukulia hatua kwa mujibu sheria kwasababu wanahatarisha maisha ya Watu”