Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Idd Kimanta amelitaka Jeshi la Polisi mkoani humo kuwakamata madereva wote wanaondesha gari huku wakiwa wamelewa na kuwaweka lupango hadi sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya zitakapopita.
Kimanta amesema hayo mkoani humo kwenye maadhimisho ya kilele cha siku 16 za kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ambapo amesema lengo la kufanya hivyo ni kupunguza ajali zitokanazo na uzembe kwa baadhi ya madereva kuendesha magari wakiwa wamelewa.
“Mkoani kwangu sitaki ajali za kizembe kuanzia sasa, RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) ninakuagiza, ukikuta mtu kalewa alafu anaendesha chombo cha moto, kamata weka ndani mpaka sikukuu zote hizi zipite, ninajua wataongea sana sababu dhamana ya haki ni ya kila mmoja, lakini uhai wa kila mtu ni mali ya serikali, hivyo lazima tuulinde kwa kukuhifadhi ndani,” Kimanta.