Maelfu ya madaktari wanaendelea kugoma kote India kudai ulinzi bora kwa wahudumu wa afya baada ya mhudumu wa afya kubakwa na kuuawa mashariki mwa jimbo la Bengal Magharibi.
Mwili wa mwanamke huyo ulipatikana Ijumaa iliyopita ukiwa na majeraha mengi na dalili za unyanyasaji wa kijinsia huko Kolkata, mashariki mwa India, polisi wa eneo hilo walisema.
Waziri Mkuu wa Bengal Magharibi Mamata Banerjee alisema alishtuka kujua daktari aliyefunzwa aliuawa hospitalini na akaunga mkono wito wa waandamanaji wa kutaka kesi hiyo ifuatiliwe haraka.
Mshukiwa mmoja amekamatwa kuhusiana na kisa hicho.
Hospitali nyingi za serikali kote India zimeacha kutoa huduma zisizo za dharura.
Mashirika ya matibabu katika majimbo mengi yalitaka kesi hiyo ifuatiliwe haraka kupitia mahakama.
Picha zilionyesha madaktari huko Kolkata wakiwa wameshikilia mabango yanayosomeka: “Wanawake maisha ya muhimu” na “Maisha ya madaktari ni muhimu pia”.
Katika mji wa kusini wa Hyderabad, madaktari walifanya mkesha wa kuwasha mishumaa.