Wanajeshi wa zamani wa Uingereza wa jinsi moja, wanaotambulika katika jamii ya LGBT, ambao walifukuzwa kutoka jeshini kwa sababu ya jinsia au utambulisho wa kijinsia, sasa wanastahiki fidia ya hadi pauni 70,000 (takriban shilingi milioni 215 za Kitanzania).
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la BBC, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza inatarajia kutangaza rasmi hatua hiyo Alhamisi, baada ya kufanya mashauriano ya kina na wanajeshi wa zamani wa LGBT pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu.
Mbali na fidia ya kifedha, mawaziri wa Uingereza wanatarajiwa kutangaza kuwa wanajeshi wa zamani wa LGBT walioathiriwa wanaweza kutuma maombi ya kurejeshewa vyeo vyao na sababu za kuachishwa kazi kwao kufanyiwa marekebisho rasmi. Serikali pia imeongeza jumla ya bajeti ya fidia kutoka pauni milioni 50 (takriban shilingi bilioni 154) hadi pauni milioni 75 (takriban shilingi bilioni 231).
Kwa mujibu wa tangazo hilo, maombi ya fidia yataanza kupokelewa Ijumaa kwa wanajeshi walioathiriwa, ambao watastahiki fidia ya awali ya pauni 50,000 (takriban shilingi milioni 154). Aidha, malipo ya ziada ya hadi pauni 20,000 (takriban shilingi milioni 62) yatatolewa kwa wale waliokumbwa na athari kubwa zaidi za marufuku hiyo, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji, uchunguzi wa kiuvamizi, au hata kufungwa gerezani.
Stephen Close, mmoja wa wanajeshi walioathiriwa, alieleza kuwa hatua hii inatoa matumaini mapya. Akiongea kuhusu mateso aliyopitia, alisema, “Kiakili, imekuwa mbaya kabisa. Nimeteseka kwa miaka mingi na unyogovu, wasiwasi, na mashambulizi ya hofu.”
Bw. Close, aliyekuwa na umri wa miaka 18 alipojiunga na jeshi, alipatikana na hatia ya kosa la ngono la aibu baada ya kumbusu mwanamume mwingine akiwa katika kituo cha Berlin katika miaka ya 1980. Aliishi kama mkosaji wa ngono aliyesajiliwa kwa miaka 30 kabla ya kusamehewa mnamo 2013.
Mpango huu unalenga kurekebisha dhuluma zilizowakumba wanajeshi wa LGBT nchini Uingereza kati ya mwaka 1967 na 2000, wakati ambapo marufuku dhidi ya wapenzi wa jinsi moja na watu wa jamii ya LGBT yalikuwa bado yanaendelea. Malipo haya yanahusisha wale waliopoteza ajira zao, walionyimwa heshima, au waliopata mateso ya moja kwa moja.