Vikosi vya Israel vilishambulia eneo la kati la Gaza kwa nchi kavu, baharini na angani siku ya Jumatano na mamlaka za Palestina ziliripoti vifo vingi zaidi, huku shirika la afya la Umoja wa Mataifa likisema maelfu ya watu walikuwa wakijaribu kukimbia mapigano.
Akionyesha azimio la Israel la kuliangamiza kundi la Hamas licha ya wito wa kimataifa wa kusitisha mapigano huku kukiwa na mzozo wa kibinadamu, mkuu wa jeshi la Israel Herzi Halevi alisema Jumanne kwamba vita hivyo vitadumu kwa miezi mingi. Hakukuwa na “njia za mkato katika kulivunja shirika la kigaidi”, alisema.
Israel pia iliashiria kuwa inaweza kuongeza kasi ya kukabiliana na mashambulizi ya mpakani kutoka kwa jirani ya kaskazini mwa Lebanon, ambako ni mshirika wa Hamas Hezbollah.
Taarifa ya wizara ya afya ya Gaza ilisema shambulizi la anga la Israel liliua Wapalestina 20 siku ya Jumatano karibu na Hospitali ya Al-Amal huko Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza. Hakukuwa na maoni ya mara moja kutoka kwa jeshi la Israeli.
Katika wilaya ya kati ya Gaza ya Al-Maghazi, Wapalestina watano waliuawa katika shambulio moja la anga, madaktari walisema, huku kaskazini mwa Gaza maafisa wa afya walisema miili ya Wapalestina saba waliouawa usiku kucha iliwasili katika Hospitali ya Al Shifa.
Wakaazi wa eneo la kati la Ukanda wa Gaza walisema usiku kucha, mashambulizi ya mizinga ya Israel yaliongezeka mashariki mwa kambi za wakimbizi za Al-Bureij na Al-Maghazi ambapo vifaru vimekuwa vikijaribu kuvuka kwa nguvu.
Jeshi la Israel siku ya Jumatano liliripoti wanajeshi watatu zaidi waliouawa katika mapigano huko Gaza, na kuleta hasara ya jumla ya kijeshi katika eneo hilo tangu operesheni za ardhini kuanza Oktoba 20 hadi 166.
Vita hivyo vilizuka baada ya Hamas kuua watu 1,200 na kuwakamata mateka 240 katika shambulio la kuvuka mpaka Oktoba 7, siku mbaya zaidi katika historia ya Israeli. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amejibu kwa shambulio ambalo limeharibu sehemu kubwa ya Gaza inayotawaliwa na Hamas.
Wizara ya afya ya Gaza ilisema wanajeshi wa Israel wamewaua Wapalestina 195 na kujeruhi 325 katika muda wa saa 24 zilizopita, na kufikisha idadi ya waliouawa hadi 21,110 na 55,243 waliojeruhiwa katika mashambulizi ya Israel katika eneo la pwani la Palestina tangu Oktoba 7.
Takriban watu wote milioni 2.3 wa eneo hilo wamefukuzwa kutoka makwao, mara kadhaa.
Huko Tel Aviv, saa kubwa ilihesabu muda uliopita tangu Hamas wachukue mateka huku familia zikiendelea na kampeni ya kutaka wapendwa wao waachiliwe.