Imeelezwa kuwa jamii inapaswa kuona na kukimbilia fursa zinazolenga kuwakutanisha na wadau mbalimbali wa maendeleo kwani kwa kufanya hivyo ndio mwanzo wa mafanikio.
Hayo yamezungumzwa leo na Mkurugenzi mwenza wa Taasisi ya Afroroots iliyopo Mkoani Iringa, Agustino Festus wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika Hoteli ya Sunset iliyopo Manispaa ya Iringa katika kikao kilicholenga kuzungumzia tukio lililoandaliwa na Taasisi hiyo la “The night of Networking msimu wa pili” likilenga kuwakutanisha wanajamii na fursa mbalimbali za maendeleo.
“Mafanikio ya maisha yanaanza kwa kukutana na watu, hivyo niwaase wanajamii ya Iringa kuja katika tukio letu kwani watakutana na wadau wengi ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara na watoa huduma mbalimbali”,
amesema Agustino. Tukio hilo linatarajiwa kufanyika Julai 27, 2024 katika Hotel ya Sunset, huku Mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa Kheri James.
Akizungumza awali Afisa wa mahusiano kwa umma wa Taasisi hiyo Irene Alphonce ameeleza kuwa tukio hilo litatanguliwa na matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutembelea kituo cha watoto yatima cha Nyumba Ali kilichopo Manispaa ya Iringa, kutembela wodi ya wazazi katika Hospitali ya Frelimo na kufanya usafi katika mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Iringa.