Wakati vita nchini Sudan vikiendelea wanawake na wasichana wamekuwa wakijifunza ujuzi mpya katika kambi ya mafunzo ya mapigano iliyoanzishwa katika uwanja wa shule wa zamani.
Mapigano ya miezi 10 kati ya jeshi la Sudan, linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah Burhan, na Rapid Support Forces, kundi lenye nguvu la kijeshi linaloongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, yameangamiza maeneo makubwa ya nchi hiyo ya kaskazini mashariki mwa Afrika.
Mzozo huo ulizuka mwezi uliopita wa Aprili katika mji mkuu, Khartoum, na kuenea haraka katika maeneo mengine ya nchi, baada ya miezi kadhaa ya mvutano unaoendelea kati ya vikosi hivyo viwili.
Katika kambi ya mafunzo huko Port Sudan, moja kati ya nyingi zilizoanzishwa nchini kote baada ya jeshi la Sudan kutoa wito kwa raia kuchukua silaha, maafisa wa kijeshi wamekuwa wakifundisha mazoezi ya wanawake na jinsi ya kutumia silaha kama vile bunduki za AK-47.
Baadhi ya wanawake waliambia shirika la utangazaji la Uingereza Sky News kuwa walikuwa wakihudhuria kambi hiyo ili kuonyesha mshikamano na wanafamilia wao ambao walikuwa wameandikishwa kupigania jeshi la Sudan.
Wengine walisema walikuwa wakijifunza ujuzi mpya wa kujilinda wenyewe na familia zao.