Mafuriko makubwa yaliyoikumba Somalia mbali na kusababisha vifu na uharibifu mkubwa yamesomba makaburi katikati mwa jiji la Galkayo na kuacha miili ikielea mitaani.
Mafuriko hayo ni mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika karne moja iliyopita.
Kuonekana kwa miili iliyofukuliwa na mafuriko kumewatisha wakazi wa mji huo hasa wanaoishi katika maeneo yaliyo karibu na makaburi.
Baadhi ya miili hiyo ilitambulika, na kuwatia kiwewe zaidi watu na maji yanapopungua mifupa iliyofukuliwa pia huonekana.
Mmoja wa wakazi wa maeneo hayo amesema, mafuriko hayo yalifichua mabaki ya mwili wa Shekhe wa Kiislamu aliyeheshimika sana na ambaye alizikwa miaka 18 iliyopita.”Wanafunzi wake na mashekhe wengine walijaribu kukusanya mabaki,” alisema, lakini hawakuweza kufanya hivyo.
Takriban watu 32 wamefariki kote nchini humo, Umoja wa Mataifa unaonya kuwa zaidi ya watu milioni 1.6 wanaweza kuathiriwa na mafuriko makubwa ambayo yanakuja baada ya nchi hiyo kukumbwa na ukame wa miaka mingi.