Kituo cha Utabiri na Matumizi ya Hali Hewa (ICPAC) cha Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) kimesema, karibu watu 270 wamefariki dunia na zaidi ya 900,000 wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua inayoendelea kunyesha katika Pembe ya Afrika.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na kituo hicho, Kenya, Ethiopia na Somalia zimeathirika vibaya zaidi na mvua za El Nino pamoja na hali ya hewa ya IOD (Indian Ocean Dipole), na idadi ya jumla ya walioathiriwa na mafurikio inakadiriwa kuwa ni watu milioni 1.5 nchini Somalia, 950,000 nchini Kenya na 101,890 nchini Ethiopia.
Zaidi ya kuhama makwao UNHCR inasema maisha ya watu yameathiriwa sana. Katika eneo moja kusini mwa Ethiopia, zaidi ya asilimia 65 ya ardhi inaripotiwa kufunikwa na mafuriko.
Wakati huo huo, zaidi ya mifugo 1,000 wamekufa, na ekari nyingine 1,000 za mazao zimeangamizwa katika mkoa wa Somalia, na hivyo kuhatarisha hali ya chakula ambayo tayari ni mbayá kuzidi kuwa mbayá zaidi.
Pia shirika hilo limeonya kwamba hali ya usafi inatia wasiwasi sana kwani mamia ya vyoo vya jumuiya vimeharibiwa, na hivyo kuwaweka watu katika hatari ya magonjwa ya kuambukiza, ikiwa ni pamoja na kipindupindu. Kwa kuongezea, barabara nyingi zimeharibiwa, na kuathiri ufikiaji wa watu kwenye huduma muhimu kama vile za afya.
Pia limesema mahitaji ya haraka ya watu kwa sasa ni “chakula, makazi ya dharura, vyombo vya jikoni, mablanketi na vitu vingine vya msaada, maji safi na huduma za usafi. Familia zinazoishi katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko pia zinahitaji msaada wa haraka ili kuhamia maeneo yenye mwinuko.”.