Hakuna mafuta yaliyosalia katika Hospitali ya al Shifa katika Jiji la Gaza, alisema daktari wa upasuaji wa Uingereza ambaye amekuwa akiwasaidia madaktari katika eneo hilo kwa miaka 15.
Hii inamaanisha kuwa hakuna viingilizi vinavyoweza kuendeshwa, wala vifaa vingine vya umeme, alisema Dk Nick Maynard.
“Hawawezi kuendesha vyumba vya upasuaji ipasavyo kwa hivyo wagonjwa wengi hawawezi kutibiwa kwa sasa na wako katika hali mbaya,” alisema.
Rafiki zake na wafanyakazi wenzake huko Gaza wanahofia kuwa watakuwa wamekufa kabla ya misaada kuwafikia, alisema.
Wamekataa kuondoka hospitalini kutokana na agizo la Israel la kuhama, licha ya kujua kuwa huenda likasababisha kifo chao, Dkt Maynard aliongeza.
Rasilimali “hazipo” na mfumo wa huduma ya afya “uko karibu kuporomoka”.
Hata kama msaada utaruhusiwa, alisema, nafasi za huduma zaidi ya matibabu ya majeraha ni “karibu haiwezekani kufikiria”, ikimaanisha wagonjwa wa saratani “watakufa tu”.
Makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani, Misri na Israel jana yalitoa taa ya kijani kwa lori 20 za misaada kuingia Gaza mara kivuko cha mpaka cha Rafah kitakapokarabatiwa. Haijulikani ni lini msaada huo utapitishwa.