Waziri wa Ulinzi Dr. Stergomena Tax leo Bungeni Dodoma amesema hali ya usalama wa mpaka kati ya Msumbiji na Tanzania ni ya wastani kutokana na mashambulizi yanayofanywa na kundi la kigaidi la Ansar Al Sunna Wal Jamaah (AASWJ) maeneo ya Kaskazini mwa Msumbiji, katika Jimbo la Cabo Delgado linalopakana na Mkoa wa Mtwara.
“Kundi hilo limekuwa likiathiri usalama kwa kuharibu na kupora mali za Wananchi, katika kupambana na changamoto hii, JWTZ imeendelea kuimarisha ulinzi kwa kufanya operesheni za ndani ya nchi na kukabiliana na kundi hilo”
“Aidha, JWTZ inashiriki operesheni chini ya Mwamvuli wa SADC nchini Msumbiji katika jitihada za kudhibiti ugaidi, operesheni hizi zimeendelea kuimarisha ulinzi katika eneo la Mpaka, kudumisha amani na utulivu, operesheni zimesaidia kupunguza nguvu ya kundi hilo la kigaidi”
“Hata hivyo, kundi hilo linatekeleza mashambulizi kwa kuhamahama na kubadili mbinu za kimapigano licha ya hali hiyo, vikundi vyetu vinaendelea kupambana kuhakikisha kundi hilo halileti madhara zaidi”