Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Jumapili alisema kwamba magaidi wasiopungua 13,000 ni miongoni mwa Wapalestina waliouawa katika vita vya Israel dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza na ameapa kuendeleza mashambulizi kusini mwa eneo hilo.
Takriban Wapalestina 31,000 waliuawa huko Gaza katika vita vya Gaza vilivyodumu miezi mitano, ambavyo vilizuka baada ya wanamgambo wa Hamas kuishambulia Israel tarehe 7 Oktoba na kuua watu 1,200 na kuwashika mateka 253, kulingana na takwim za Israel.
Wizara ya afya ya Gaza haitofautishi idadi ya vifo kati ya raia na wanamgambo wa Hamas lakini ilisema kwamba asilimia 72 ya wale waliouawa ni wanawake na watoto. Hamas imetupilia mbali takwimu hizo za Israel na kusema ni njama ya kudai “ushindi bandia”.
Netanyahu alikiambia chombo cha habari cha Ujerumani Axel Springer, mmiliki wa magazeti ya Politico na Bild na kituo cha televisheni cha Welt, kwamba kuendeleza mashambulizi ndani ya Rafah kusini mwa Gaza ni muhimu sana kuishinda Hamas.