Vigogo wizara ya kilimo, chakula na ushirika akiwamo Katibu mkuu Sophia Kaduma, wametimuliwa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) baada ya kutoa majibu yasiyoridhisha kuhusiana na hati waliyopewa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alihoji kuhusiana na sababu iliyofanya vigogo hao kutoa vibali kwa kuingiza mchele kutoka nje ya nchi huku wakulima wa nchini wakiwa wamezalisha zao hilo kwa wingi, na pia kuhusiana na deni la shilingi bilioni 4 linalotokana na mauzo ya mbolea ya Minjingu.
Mbali na mambo hayo, Zitto alihoji pia kuhusu namna ambavyo wamejipanga kuwatafutia soko wakulima wa mahindi, ambapo Kaduma alijibu wizara inatoa vibali vya kuuza mazao ya mahindi na mchele nje ya nchi na hana taarifa kama kuna mazao yanayoingizwa nchini, jambo lililowakasirisha wajumbe wa kamati ya PAC na kuhoji wao kama wahusika kwa nini wasijue kama kuna uingizwaji wa mazao hayo nchini.
Kuhusiana na suala la hati isiyoridhisha ya CAG, Kaduma amekiri kukosekana kwa nyaraka za deni la shilingi bilioni 2.1 lililotokana na udhaifu wa utunzaji wa nyaraka kutokuwa mzuri.
MWANANCHI
Vipimo vya mgonjwa aliyetoka nchini Senegal na kuwekwa karantini mjini Moshi kwa tahadhari ya Ebola , vimepelekwa katika maabara jijini Nairobi, Kenya kwa uchunguzi.
Hayo yamesemwa na mganga mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Mtumwa Mwako wakati uongozi wa wa mkoa wa Kilimanjaro ulipokutana na wanahabari kutoa taarifa ya maendeleo ya uchunguzi wa awali ambapo amesema madaktari na wauguzi wanaomhudumia mgonjwa huyo nao wamewekwa karantini kusubiri majibu ya vipimo hivyo.
Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Leonidas Gama amewatoa hofu wananchi wa mkoa huo na kuongeza kuwa maeneo aliyopita mgonjwa huyo wameyabaini na kuchukua tahadhari.
Kwa upande wake mganga mkuu Dk. Mwako amesema mgonjwa huyo ametoa ushirikiano mkubwa na wamepata rekodi ya magari aliyopanda akiwa nchini ili ikitokea majibu yamekuja tofauti watajua namna ya kufanya.
MWANANCHI
Timu ya wataalamu wa kimataifa imegundua aina mpya ya viumbe jamii nyoka, mijusi na vyura ambavyo havipatikani sehemu nyingine duniani katika Milima ya Tao la Mashariki nchini Tanzania.
Akizungumzia ugunduzi huo mkurugenzi wa Shirika la Uhifadhi wa Misitu ya Asili Tanzania Charles Meshack amesema ugunduzi huo unaifanya Tanzania kuwa jumla ya aina 211 ya viumbe vya aina ya pekee.
Meshack ameiomba serikali kuingiza milima hiyo katika mchakato wa urithi wa dunia ambapo itasaidia kuitambulisha kimataifa na kuinufaisha nchi kupitia utalii.
MWANANCHI
Jumla ya wanafunzi 5 tu ndio waliofanikiwa kuhitimu kidato cha nne shule ya Sekondari ya Kata ya Membe, Wilayani Chamwino Dodoma.
Akisoma risala katika mahafali ya tatu ya shule hiyo mwanafunzi Livingstone Samwel amesema walianza kidato cha kwanza wakiwa wanafunzi 18, kati yao wasichana walikuwa sita.
Baadhi ya sababu zilizotajwa kuchangia wanafunzzi wengine kushndwa kuhitimu kuwa ni pamoja na utoro, mwamko mdogo wa wazazi, msongamano wa wanafunzi katika vyumba vya madarasa, upungufu wa walimu na ukosefu wa nyumba za walimu unapelekea utoro wa walimu.
Mgeni rasmi wa katika mahafali hayo Godrick Ngoli kutoka chuo cha mipango na Maendeleo (IRDP) amewata wanafunzi hao kusoma kwa bidii, na kuwahimiza wazazi kuwapeleka watoto walioshindwa kuendelea na masomo katika vyuo vya ufundi.
MTANZANIA
Mtandao hatari unaojihusisha na matukio ya ujambazi wa kutumia silaha umebainika, ambapo uchunguzi uliofanywa na gazeti la MTANZANIA umebaini kuwepo kwa mtandao mpana unaotekeleza uhalifu huo.
Mtandao huo unaohusika na uharamia kwenye benki unawahusisha baadhi ya askari polisi, wafanyakazi wa benki, madereva wa bodaboda na magenge ya ujambazi.
Katika uchunguzi huo inaonekana baadhi ya watumishi katika benki wameingizwa katika mtandao kwa ajili ya kutoa taarifa za wateja wanaochukua kiasi kikubwa cha fedha.
Kamishna Suleiman Kova amesema wapo polisi wanaoshiriki matukio hayo na sio jeshi lote, na kuongeza kuwa wapo watumishi katika mabenki wanaoshirikiana na majambazi katika uhalifu huo, hivyo kushauri taasisi hizo kufanya uchunguzi na kushirikiana na jeshi la Polisi ili kuwabaini.
MTANZANIA
Mratibu wa Makaburi na Mazishi Dar es Salaam Nasibu Rashid amesema jiji la Dar es Salaam huzika wastani wa maiti 15 zisizokuwa na ndugu, vichanga waliofariki baada ya kuzaliwa, au wasiokuwa na uwezo kufanya mazishi kila mwaka, ambapo kwa mwezi wamekuwa wakizika maiti kati ya 30 na 40.
Amesema maiti wanazozika zinatoka hospitali ya taifa Muhimbili, Mwananyamala, Temeke, Ocean Road, Amana, Vijibweni, na nyingine kutoka Zahanati za Manispaa za jiji ambapo maiti hizo ni zile zilizokaa hospitalini kwa zaidi ya wiki 2.
Naye Mganga Mkuu Hospitali ya Manispaa ya Kinondoni amesema maiti nyingine zinazozikwa zinaletwa na jeshi la polisi kutokana na vifo vinavyotokana na ajali za barabarani.
HABARI LEO
Tume ya taifa ya uchaguzi (NEC) imetangaza kuanza maboresho ya Daftari la Wapgakura kuanzia mwezi ujao na kukamilika April 18, dalili zinazoonesha zoezi la upigaji kura ya maoni katiba mpya iliyopendekezwa kuanza siku chache baada ya zoezi hilo kukamilika.
NEC wamekuwa na wasi wasi huenda zoezi hilo lisikamilike kwa wakati kutokana na serikali kutowapatia fedha kiasi cha sh. bilioni 293, lakini kwa upande wake Naibu katibu mkuu wa tume hiyo Sisti Caria amesema matumaini yaliyopo ni makubwa kulikamilisha zoezi hilo kwa wakati na kufikia Aprili watakuwa wameandikisha wapigakura mil. 23.9.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema mchakato huo haujawapa taarifa rasmi wadau wa vyama vya siasa na wamekuwa wakipata taarifa kuhusiana na hilo kupitia vyombo vya habari.
HABARI LEO
Tume ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kazi (CMA) imetoa siku 90 kwa lililokuwa Shirika Hodhi la Reli (RAHCO) ambalo lilikuwa likihodhi mali zilizokuwa chini ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), kuwalipa waliokuwa waajiriwa wa TRC kabla ya mkataba wa wao na shirika hilo kukoma.
Mwenyekiti wa wa Tume hiyo Anosisye amesema, maamuzi hayo yametoka baada ya kupitia nyaraka zilizowasilisha napande hizo mbili na kubaini kuwa RAHCO inawajibika kuwalipa mafao hayo ya kustaafu.
Wastaafu hao wanaidai RAHCO jumla ya sh. bilioni 16.2, mafao ambayo yalipaswa kulipwa na TRC na baadaye kuachwa mikononi mwa RAHCO.
Aidha wastaafu hao wamesema wameamua kufungua mashauri ya madai hayo tume ya Usuluhishi baada ya kupigwa danadana na RAHCO na TRL, ambao kila mmoja alionekana kuyapinga madai yao.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook