Leo March 16, 2018 Vigogo watano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la matumizi mabaya ya madaraka.
Washtakiwa hao ni Mkurugenzi Mtendaji, James Mataragio, Kaimu Meneja wa uvumbuzi, George Seni, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na utawala, Wellington Hudson, Mkurugenzi wa Mkondo wa Juu, Kelvin Komba na Edwin Riwa ambaye ni kaimu Mkurugenzi wa mipango.
Mwendesha mashtaka wa TAKUKURU, Emmanuel Jacob amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu,Wilbard Mashauri kuwa washtakiwa wametenda kosa hilo kati ya April 8, 2015 na June 3,2016.
Inadaiwa wakiwa watumishi wa umma na waajiriwa wa TPDC kwa nafasi zao, wakati wakitimiza majukumu yao kwa makusudi walitumia madaraka vibaya.
Inadaiwa walibadilisha na kupitisha bajeti na mpango wa mwaka wa manunuzi wa mwaka 2014/2015 na 2015/2016 kwa kuingiza ununuzi wa kifaa cha utafiti cha airborne gravity gradiometer survey ndani ya ziwa Tanganyika bila ya kupata kibali cha bodi ya wakurugenzi ya shirika.
Inadaiwa kitendo hicho kinakiuka kifungu cha 49(2) cha sheria ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 kwa lengo la kujipatia manufaa yasiyohalali ya Dola Milioni 3,238,986.50 ambazo ni sawa na (Sh.Bilioni 7.2) kwa Bell Geospace.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa wote walikana na upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Hakimu Mashauri alitoa masharti ya dhamana kwa washtakiwa ambapo wametakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini bondi ya Sh.Bilioni 1 ambapo wametimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana. Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi March 19, 2018 kwa ajili ya kutajwa.