Waendesha mashtaka wa Afrika Kusini watawasilisha hoja za mwisho katika ombi la dhamana la wanaume watano wanaoshtakiwa kwa mauaji ya mwanamuziki Kiernan “AKA” Forbes na rafiki yake Tebello “Tibz” Motsoane katika Mahakama ya Durban siku ya Ijumaa.
Wawili hao walipigwa risasi na kuuawa nje ya mkahawa mmoja wa Durban mwaka jana, na kuibua mshtuko mkubwa kutoka kwa mashabiki wa muziki barani humo na jumuiya kubwa ya muziki.
Washtakiwa watano, Lindokuhle Mkhwanazi, Lindani Ndimande, Siyanda Myeza, Mziwethemba Gwabeni na Lindokuhle Ndimande, walikuwa mahakamani hapo Alhamisi wakati mawakili wao wa utetezi wakihitimisha hoja zao za mwisho katika ombi la dhamana.
Washukiwa wengine wawili, Siyabonga na Malusi Ndimande, wako kizuizini huko eSwatini wakisubiri ombi la kurejeshwa nchini Afrika Kusini, SABC inaripoti.
Mnamo Februari, polisi walisema waliwakamata washukiwa sita baada ya kufanya uchunguzi kwa karibu mwaka mmoja.
Afrika Kusini ina moja ya nchi zenye viwango vya juu zaidi vya mauaji duniani, huku kukiwa na nyota kadhaa za burudani miongoni mwa wahasiriwa.
Mnamo mwaka wa 2007, mwimbaji wa reggae Lucky Dube alikuwa akimshusha mtoto wake wa kiume kwenye nyumba ya jamaa yake wakati watu wenye silaha walipompiga risasi mara tatu wakati wa jaribio lisilofaulu la kuiba gari lake.