MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, imeeleza utayari kushirikiana na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) wa kufanyia marekebisho baadhi ya sheria zinazohusu masuala ya fidia, ili kuboresha huduma za fidia kwa walengwa, Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe, Dkt. Yose Joseph Mlyambina, amesema.
Mhe. Dkt. Mlyambina, amesema hayo jijini Arusha, kwenye Kikao Kazi baina ya WCF na Majaji wafawidhi, Majaji wa Kanda, Watendaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi pamoja na Watendaji wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), jijini Arusha, Disemba 2, 2023.
“Naamini tutaendelea kuiboresha kwa kina, sheria yetu, kwa manufaa yetu sisi kama Watanzania, sisi waheshimiwa majaji, waheshimiwa manaibu wasajili na wasuluhishi wote, tuko tayari kutoa mawazo yetu kutokana na uzoefu tunaoupata kazini, kwa ajili ya kuboresha sheria yetu ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.” Alifafanua Dkt. Mlyambina.
Amesema, anatamani WCF iwe mfano wa kuigwa sio tu Barani Afrika bali Duniani kote katika masuala ya Fidia kwa Wafanyakazi na kuishukuru Bodi ya Wadhamini ya WCF, kwa kuisimamia vema taasisi hiyo.
“Hakika wanatekeleza vema majukumu yao kwa faida ya Watanzania, mtakubaliana nami, elimu tuliyoipata hapa ina mchango mkubwa sana katika kuiboresha sheria ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, na hii sio tu kwamba ina manufaa kwa Mfuko, bali kwa Watanzania wote.”Amesema Jaji Mlyambina.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Revocat Mteule, amesema WCF ina faida kubwa sana kwa wafanyakazi na kwakuwa sheria zinaendelea kuboreshwa, ana mataumaini makubwa kuwa Wafanyakazi watanufaika zaidi na Mfuko.
“Rai yangu mimi leo ni kwa waajiri, kuona umuhimu huo, kwa sababu sio kwa faida ya mfanyakazi peke yake, inapotokea mfanyakazi ameumia kazini, huo ni mzigo wako lakini badala ya kubeba mzigo huo, tambua kwamba WCF ipo na jukumu lake ni kumuhudumia mfanyakzi aliyepatwa na changamoto akiwa kazini.” Amesema, Mhe. Mteule.
Naye Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Bw. Usekelege Mpulla, amesema, Kikao Kazi hicho kina manufaa makubwa kwani wote kazi yao ni kuwahudumia waajiri na waajiriwa.
“Yapo baadhi ya mashauri yanakuja kwenye Tume, lakini kwa yale mashauri ya kuumia kazini, yanaweza kuhudumiwa na WCF, hivyo CMA inabadilishana taarifa na WCF na hivyo kuwawezesha wananchi kuhudumiwa kwa wakati.” Alifafanua.