Mahakama katika mji mkuu wa Ghana Accra imewahukumu wanachama wanne waandamizi wa chama cha Magharibi cha Togoland Restoration Front (WTRF), kikundi kinachotaka kujitenga, kifungo cha miaka 17 jela kwa kuendesha shirika lililopigwa marufuku.
Hukumu yao Jumatano inajiri baada ya Jaji Mary Maame Ekueh Nyanzuh wa Mahakama Kuu ya Accra kuwapata wanne hao na hatia ya makosa kadhaa.
Wafungwa hao ni pamoja na maafisa wa zamani wa polisi na wanajeshi.
Mashtaka yaliyotolewa dhidi yao yalikuwa: kuwa wanachama wa shirika lililopigwa marufuku, kuitisha mikutano ya shirika lililopigwa marufuku, kuhudhuria mikutano, na kutoa michango kwa manufaa ya shirika lililopigwa marufuku.
Mwanzilishi wa WTRF, Michael Koku Kwabla, almaarufu Togbe Yesu Edudzi, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela, na faini ya cedis 12,000 za Ghana ($940).
Washukiwa wengine watatu Nene Kwaku, Emmanuel Afedo, na Abednego Mawena walihukumiwa kifungo cha miaka minne jela kila mmoja, na faini ya cedis 4,800 ($375) kila mmoja.
Wakili wa utetezi Andy Vortia aliomba wateja wake wapewe adhabu nafuu, akisema tayari walikuwa wamekaa rumande kwa miaka mitatu.
Upande wa mashtaka, ukiongozwa na Joshua Sackey, ulipinga ombi hilo la hukumu fupi, ukiiomba mahakama kutoa adhabu kali ili kuwazuia wanaotaka kuwa wahalifu.