Mahakama ya Juu ya Chad jana Alkhamisi ilitangaza kuwa katiba mpya iliyopitishwa katika kura ya maoni tarehe 17 Disemba 2023 kwa asilimia 85.90 ni halali na imepasishwa na mahakama hiyo.
Tume ya Taifa Iliyosimamia Kura ya Maoni ya Katiba hiyo ilitangaza wakati wa kutoa matokeo kwamba, zaidi ya asilimia 63 ya ya wananchi milioni 8.3 wa Chad waliotimiza mashari ya kupiga kura walishiriki kwenye kura hiyo ya maoni ya Disemba 17.
Hatua inayofuatia sasa ni kwa rais wa mpito wa nchi hiyo, Mahamat Idriss Deby Itno, kutia saini na kutangaza rasmi katiba mpya ili kuweka mazingira ya kufanyika uchaguzi mwakani na kurejea utawala wa kiraia huko Chad.
Hali ya kisiasa na kijeshi nchini Chad ni mbaya tangu mwaka 2021 kufuatia mauaji ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Idriss Deby Itno. Tngu baada ya kuuawa baba yake, Mahamat Idriss Deby Itno ndiye anayeongoza Chada kupitia baraza la mpito la kijeshi.
Viongozi wa kijeshi wa Chad wameitaja kura hiyo kuwa ni hatua muhimu kuelekea kwenye utawala wa kidemokrasia baada ya jeshi kutwaa madaraka mwaka 2021 wakati rais wa zamani wa nchi hiyo, Idriss Deby, alipouawa kwenye uwanja wa vita katika mapigano na waasi.
Katiba hii mpya itaidumisha serikali ya umoja wa kitaifa, ambayo Chad imekuwa nayo tangu ilipopata uhuru, na itaanzisha jamii zinazojitegemea na mabaraza ya mitaa na machifu wa kimila miongoni mwa mabadiliko mengine.