Mahakama ya kijeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imewahukumu kifo watu 26 wanaotuhumiwa kuhusika na makundi yenye silaha, wakiwemo wa M23 baada ya kesi iliyoanza mwishoni mwa mwezi uliopita.
Corneille Nangaa, kiongozi wa Alliance Fleuve Congo (AFC) alipatikana na hatia ya uhalifu wa kivita, kushiriki katika uasi na uhaini.
Nangaa na washitakiwa wengine 20 walihukumiwa kifo bila kuwepo mahakamani siku ya Alhamisi, kwa kuwa kwa sasa wako mbioni.
Washtakiwa watano waliohudhuria kesi hiyo wana siku tano za kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo, rais wa mahakama hiyo alisema.
Mwendesha mashtaka katika kesi hiyo iliyoanza Julai 24, alitoa wito wa hukumu ya kifo dhidi ya washtakiwa 25 na kifungo cha miaka 20 jela kwa mshtakiwa mmoja.
Nangaa, rais wa zamani wa tume ya uchaguzi ya DRC, alizindua vuguvugu la kisiasa na kijeshi la AFC mwezi Disemba kwa lengo la kuunganisha makundi yenye silaha, vyama vya siasa na jumuiya za kiraia dhidi ya serikali.
Mmoja wa wanachama wake ni kundi lenye silaha la M23 linalotuhumiwa kwa mauaji ya halaiki katika mzozo wa miongo kadhaa mashariki mwa DRC.
Wahusika wakuu wa M23 walioshtakiwa ni pamoja na rais wake Bertrand Bisimwa, mkuu wa jeshi Sultani Makenga na msemaji Willy Ngoma na Lawrence Kanyuka.